.

.

.

.

Wednesday, 21 June 2017

FAHAMU JINSI YA KULIMA UYOGA NA FAIDA ZAKE KATIKA MWILI WA MWANADAMU

FAHAMU JINSI YA KULIMA UYOGA NA FAIDA ZAKE KATIKA MWILI WA MWANADAMU


 
UTANGULIZI.
 
Uyoga ni aina ya nyuzi kuvu (fungus) yenye kutofautiana na mimea mingine kwa kukosa chembe chembe zinazowezesha mimea kujitengenezea chakula yenyewe kwa kutumia hewa na mwanga.
Uyoga unaota wenyewe kwenye mashamba hasa wakati wa mvua kwenye maeneo yenye mboji nyingi. Sasa hivi nchini tunao utaalamu wa kuotesha uyoga au ndani ya nyumba au nje kwenye kivuli maalumu.

 
HISTORIA FUPI YA UYOGA.
Uyoga umefahamika na wanadamu tangu enzi za zamani sana. Miaka elfu nne kabla ya kuzaliwa Kristo watu walijua uyoga. Historia inatueleza kwamba watu wameanza kulima kwa utaalamu mwaka 300 baada ya kuzaliwa Kristo.
Wadadisi wa mambo wanauelezea Uyoga kufanana sana na chakula waisraeli walichokuwa wakila kule jangwani katika safari yao ya kutoka utumwani Misri.
Wakati Uyoga ukilimwa katika dunia yote, hapa Afrika na hasa kwetu Tanzania mambo yalikuwa ni tofauti kabisa. Hakuna mtu aliyesumbuka na kilimo hicho. Ni hapo majuzi tu mwaka 1993 ndipo ukulima ulianza Dar es salaam. Mwaka 1994 ukulima ulianza Arusha, mwaka 1995 ukulima ulianza huko Mbeya, na mwaka 2003 ukulima ulianza huko Kilimanjaro.

 
AINA YA UYOGA.

 
Inakadiriwa kuwa kuna aina milioni moja na laki tano (1,500,000) za nyuzi kuvu (fungus) duniani; katika hizi ni aina 64,000 ambazo zimekwisha kufanyiwa utafiti na kupatiwa maelezo ya kisayansi. Katika hizi aina 64,000, kuna ambazo zimethibitika kuwa na Uyoga halali 12,000. Na kati ya hizi ni aina 2,000 na ndizo zinazolimwa.
Katika aina 2,000 za uyoga zilizokwisha thtbitika, hapa Tanzania ni aina 40 tu.
Uyoga Mamama (Oyster mushroom).
Aina hii ya Uyoga hustawi katika nchi za Tropics. Utaalamu unaohitajika siyo mgumu. Baadhi ya aina zinazooteshwa ni hizi zifuatazo;
. Pleurotus oystreotus
. Pleaurotus sajo-caju
. Pleaurotus sapidus
. Pleurotus flabel atus - (pink oyster)
. Leaurotus Pulmonerius
. H. K. n.k
. Monkey Head
. Auriclaria
Nyingine zinazooteshwa hapa nchini kwa kiasi kidogo ni;
. Agaricus bitoquis (uyoga vifungu)
Uyoga taka ambazo ni;
. Coprinus cinereus
. Caprinus Comatus
. Lentinus edodes
. Volvoriella Volvocea
Nyingine ni;
. Ganodema lucidum

 FAIDA ZA UYOGA
Uyoga una maajabu makubwa katika maisha ya mwanadamu, Uyoga ni lishe bora kwa mwanadamu, ni dawa na tiba kwa mwanadamu, ni zao la kuingizia watu kipato, ni rafiki wa mazingira pia.
LISHE
. Uyoga ni zao lenye viini lishe (amino acids) zote 22 zinazohitajika na mwili wa mwanadamu.
. Protini iliyoko kwenye Uyoga inafikia kiwango cha asilimia arobaini. Hii inalingana na protini iliyoko kwenye maziwa.
. Kuna wingi mkubwa sana wa vitamini B,C na D.
. Uyoga hauna mafuta mengi. Una asilimia tatu tu. Hivyo hauna Colestrol.
. Uyoga unayo madini yote muhimu kwa mwanadamu; phosphorus, Iron, Calcium na Potash.
TIBA
Utafiti uliofanyika siku za karibuni umethibitisha kuwepo kwa dawa nyingi ndani ya uyoga zenye uwezo wa kutibu kwa ufanisi, magonjwa ya wanadamu na mifugo. Kwa wanadamu magonjwa yafuatayo yanatibiwa;
. Kifua kikuu TB
. HIV/AID upungufu wa kinga mwilini
. Kisukari
. Shinikizo la damu
. Magonjwa ya moyo na uti wa mgongo
. Saratani
. Matatizo ya figo
. Vifo vya watoto wachanga
AJIRA
Kwa sasa hivi ajira imepungua sana katika nchi yetu. Vijana, wazee na rika lote hatuna kazi, mazao yaliyokuwa yakituingizia kipato yamepungua au yamekwisha. Nguvu kazi nyingi tuliyonayo inatumika kuuza mwanasesere na plastic zinazotoka katika nchi za nje.
Watu wengi mno tunaishi katika lindi la ufukara. Hatuna mahitaji ya msingi kama vile chakula, malazi na mavazi bora. Kufuatana na ripoti ya umoja wa mataifa, iliyoandaliwa na Professors S. T. Chang na Mshigeni wa chuo kikuu cha Namibia, mauzo ya Kahawa kwenye soko la ulimwengu kwa mwaka 1997 ni dola za kimarekani bilioni 15. Mauzo ya Uyoga yalikuwa dola bilioni 14. Katika biashara hiyo Afrika ilichangia kwa asilimia 0.3 tu.
Wataalamu hawa wanaainisha sababu nyingi zinazosababisha upungufu huu. Kubwa wanalosema ni kuwa waafrika hawajui umihimu wa uyoga katika maisha ya mwanadamu. Bei ya uyoga huko Marekani, Mashariki ya kati na Mashariki ya Mbali ni kati ya dola za Marekani tisa ($9) hadi kumi na tatu ($13). Uyoga ni zao lililo kayika mpango nafuu wa biashara ya Marekani na Afrika. Halitozwi ushuru kuingia katika masoko ya Marekani.


 
KUSAFISHA MAZINGIRA
Kufuatana na ripoti ya wataalamu wa chuo kikuu Kivais na Magingo ya miaka ya tisini, Tanzania inayo masalio ya kilimo na misitu zaidi ya tani milioni kumi na saba (17,000,000). Masalio haya yameachwa yakioza, au kuchomwa moto au kulishwa mchwa pamoja na mapanya. Ikiwa masalio haya yatatumika kuoteshea Uyoga, Mazingira yataboreka na uchumi utakua. Uzalishaji wa Uyoga unaanzia pale mkulima au mtumiaji wa bidhaa za kilimo na misitu anapomalizia.

 
MASALIO YA TAKATAKA BAADA YA KUOTESHA UYOGA.
Masalio ya takataka (vimeng'enywe) hutumika kama ifuatavyo;
. KULISHA MIFUGO
Uyoga una uwezo wa kuvunja vunja chembe chembe za vimeng'enywe na kuviboresha kuwa protini na madini mengi, kisha kufyonza hicho na kutengeneza matunda ya uyoga. Baada ya kuvuna uyoga chembechembe hizi bado zina ubora mkubwa wa chakula kwa ajili ya mifugo kama vile ng'ombe, mbuzi, nguruwe, sungura n.k. Tunao wafugaji wanaotumia vimeng'enywe hivi kulishia mifugo nao wameendelea kupata maziwa mengi.
. MBOLEA
Vimeng'enywe hivi hutumika kama mbolea shambani na katika bustani. Matokeo ya kutumia vimeng'enywe hivi yameonyesha ufanisi mkubwa.
.METHANE GAS
Tukijenga mfumo wa kutengeneza gesi kama kawaida, tunaweza kutumia vimeng'enywe hivi kutengeneza methane gas. Hii gesi itatumika kupikia, kuwasha taa na mambo mengine kama hayo. Mabaki katika zoezi hili huwa na mbolea nzuri ifaayo sana. Mazao ya shamba na bustani yaliyokuzwa kwa mbolea hii yana bei nzuri zaidi sokoni, maana yanahesabika yamezalishwa kiasili (organic agriculture).
. ZERI ( Zero Emmission Research Initiative).
Umoja wa Mataiga umeiteua Tanzania pamoja na nchi nyingine katika bara la Afrika kuendeleza na kutekeleza mfumo wa ZERI. Huu ni mfumo wa kutochafua mazingira kwa njia ya kutoa moshi. Masalia ya kilimo ba misitu yasichomwe moto bali yageuzwe kutoka hali yake na kuwa kitu kingine labda kilicho bora na chenye thamani zaidi. Masalia ya sokoni hatutayaacha yaoze bure, tutayasindika ili yaweze kuzalishia uyoga. Pumba za mpunga na kahawa hatutazichoma moto. Tutazitumia kwa kuzitengenezea chipboards, vivyo hivyo na maranda ya mbao, takataka za katani, kahawa na n.k. zitageuzwa kuwa kitu bora zaidi.
 
UTAYARISHAJI WA SHAMBA LA UYOGA.
Mambo ya muhimu ya kuzingatia:
. Ukubwa wa shamba
. Uwezekano wa upanuzi
. Usafi wa eneo
. Upatikanaji wa takataka za kulimia yaani vimeng'enywe 
. Upatikanaji wa maji safi
. Umbali kutoka kwenye soko
Ndani ya ndani
. Hewa safi ya inayozunguka
. Joto linalotakiwa
. Unyevunyevu kwenye hewa unaotakiwa
. Carbondioxide na mwanga vinatakiwa
Shamba
Shamba la uyoga linapaswa liwe na viambatanisho vifuatavyo;
. Sehemu ya kutayarisha vimeng'enywe
. Kichanja cha kuhifadhi majani au aina yoyote nyingine ya vimeng'enywe.
. Sehemu ya kuchemshia vimeng'enywe

. Sehemu ya kupandia mbegu kwenye vimeng'enywe vilivyokwisha kuchemshwa.
. Banda kamili la kukuzia lenye sifa zilizokwisha ainishwa hapo juu
. Sehemu ya kuhifadhia uyoga uliovunwa au chumba cha baridi kutegemea na hali halisi.

 
UJENZI WA SHAMBA
Mkulima anashauriwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika eneo lenyewe. Kwa mfano mkulima mwenye shamba la migomba, baai atumie marawa katika kuta na paa. Unaweza ukatumia nyasi za kawaida au majani ya mpunga, ngano na mengine ya namna hiyo, unaweza kutumia matofali mabichi, unaweza kutumia mabanzi. Ndani ya nyumba weka weupe. Hii ni chokaa au kitambaa cheupe. Hii ni kwa sababu uyoga hukua kuelekea rangi ya mazingira yaliyouzunguka. Lakini rangi nyeupe huchochea ukuaji na hudumisha usafi. Nyumba ya uyoga iwe na madirisha makubwa mazuri.

 
MAANDALIZI YA VIMENG'ENYWE
Kama ilivyosemwa hapo mwanzo, kila jani lililokomaa na kukauka, lafaa kuoteshea uyoga. Michanganyiko ifuatayo yafaa sana kuoteshea uyoga.
. Majani ya mpunga au migomba yenye unyevu 62%
. Pumba za mahindi unyevu 62%
. Sukari
. Chokaa
Vimeng'enywe viko vingi, mkulima anashauriwa awaone wataalamu kwa ushauri.
MAHITAJI MENGINE
Ifuatayo ni orodha ya mahitaji mengine;
. Jiko la kuchemshia
. Pipa tupu la lita mia mbili
. Mifuko ya plastic size 10" × 15" yenye uwezo wa kuhimili joto
. Viroba (polysacks) pvs ya kuweka ndani ya pipa
. Vibangili vya kipenyo cha 1.5
. Kamba au uzi wa kushonea viatu ili kufunga mifuko wakati wa kuchemsha.
. Vipande vya magazeti
. Rubber band size ya mpira wa ndana ya tairi ya baiskeli.

 
HATUA ZA KUFUATA KATIKA KUOTESHA
. Katakata majani yaliyokomaa na makavu katika urefu usiozidi nchi nne
. Changanya majani haya na virutubisho hapo juu i.e. pumba za mahindi, sukari na chokaa.
. Changanya sawasawa kwa kutumia maji safi ndoo tatu hadi tano.
. Zilundike mahali safi ukitengeneza mlinduko wenye kimo cha mita moja hadi mita moja na nusu.
. Funika kwa polythene paper na vitambaa vya sulphate 
. Majani ya migomba yalowekwe kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuvundikwa
. Ziache kwa muda wa masaa 24
. Weka vimeng'enywe hivi katika mifuko ya polythene
. Weka maji lita 40 katika pipa lenye kichanja cha mbao chenye kuzuia mifuko isigusane na maji
. Bandika kwenye jiko hadi mvuke unapotoka , hesabu msaa manne.
. Ipua mifuko yako na iweke mahali safi
. Sasa ni wakati wa kufanya kila kitu kwa hali usafi. Tunatumia maji yenye detol kusuzia mikono yetu
. Otesha uyoga kama mtaalamu atakavyokuonyesha
. Baada ya siku 21 ondoa vipande vya gazeti ulivyotumia kufunika mifuko
. Baada ya siku 10 nyingine utaanza kuvuna uyoga. Uta una kwa muda wa miezi 2 hadi 3
. Weka uyoga uliovuna ili kuhifadhi ubora wa uyoga.
MAPATO YA MKULIMA
Tunaorodhesha hapa hali halisi ya mkulima wetu mwenye banda la mita tatu (3) kwa mita tano (5).
Gharama:
Majani ya mpunga Pickup moja = 25,000/-
Mifuko ya plastic 500@50 = 25,000/-
Mbegu za uyoga chupa 100@1500 = 150,000/-
Jumla = 200,000/-

Mavuno aliyopata kilo 300@3000 = 900,000/-
Toa gharama = 200,000/-
Salio = 700,000/-
Kazi hii ilimchukua mkulima huyu miezi mitatu. Ijulikane kuwa baada ya kuotesha mkulima anakagua banda kw muda mfupi sana, asubuhi saa sita na jioni. Mkulima huyu na familia yake anajipatia wastani wa shilingi 230,000/- kila mwezi kwa kulima banda moja.
MAPISHI
Mkulima na umma wote wanapashwa kujua mapishi ya uyoga. 
Tunaweza kutumia uyoga kama ifuatavyo;
. Kutengeneza supu
. Kutengeneza supu ya viungo (mushroom curry) 
. Kutengeneza mboga ya kawaida tunayoweza kula na vyakula vingine kama vile ugali ndizi, wali, viazi n.k.
. Tunaweza kuzindika a kutengeneza mushroom pickle (hii tutauza kwenye supermarket na mahoteli ya kawaida hasa ya kitalii)
. Tunaweza kutengeneza mushroom pizza.

 
MAGONJWA YA UYOGA
Uyoga ni viumbe hai. Hivyo hupatwa na magonjwa kama hali ya mazingira na utendaji haitakidhi. Kuna magonjwa ya aina kama ifutavyo;
. Bacteria
Uyoga unakuwa na rangi ya kutu. Hata mifuniko inakuwa na rangi hiyo. Ugonjwa huu unatambulika kiurahisi., kwani unakuwa unateleza.
. Fungus
Aina zifuatazo ndizo hasa zishajulikana;
. Blue mould
. Black mould
. Brown mould
. Virus
Uyoga uliopendeza unasinyaa mara moja. Unaanza kutoka jasho.

 
MASOKO
Mpaka sasa hoteli za kitalii zinapika uyoga wa kutoka nje uliowekwa kwenye makopo. 
Ikumbukwe kuwa kwenye makopo kuna uyoga halisi kidogo sana. Pia katika supermarket za hapa nchini kuna uyoga fresh kutoka Kenya. Pia tujue kuwa majirani wetu waliotuzunguka Kenya, Uganda, Zambia na Malawi wamepiga hatua kubwa katika kilimo cha uyoga. Swali tunalopaswa tujiulize sote ni hili " Kulikoni Tanzania kuhusu Uyoga".
Tumeziona faida za uyoga. Ni bora kuliko nyama nyekundu na nyama nyeupe. Kwenye maduka ya nyama zinauzwa kilo nyingi za nyama kila siku. Badala yake tuuze uyoga kila siku.

 
SOKO LA NJE
Kama ilivyoelekezwa hapo juu kuna masoko ya nje. Lakini yanataka kiasi kikubwa cha uyoga. Tani kadhaa kila wiki na kila mwezi. Ili kuweza kukidhi haja hii, wakulima waunde vikundi na vyama vya ushirika ili kushughurikia jambo hili.

 
HITIMISHO
Andiko hili dogo lina lengo la kumuandaa Mtanzania wa kawaida aweze kuwa mkulima wa uyoga. Kamwe lisichukuliwe kama mamlaka tosha kuhusu uyoga. Sababu ni kwamba nimechagua kuzungumzia yale mepesi tu yanayoweza kumfaa mkulima wa ngazi ya mwanzo. Sayansi ya uyoga ni pana, ndefu na yenye kina.
Ahsanteni sana.
Imeandaliwa na kuandikwa na Marcodenis E. Misungwi,
Mtaalamu wa Kilimo na Mifugo III, Mbozi District Council
Kwa msaada wa International Fund for Agricultural Development, IFAD
Share:

HII NDIO RATIBA YA CHANJO ZA KUKU

RATIBA ZA CHANJO KWA KUKU

CHANJO ZA KUKU - RATIBA MAALUM

1.     SIKU 1. 
 Baada ya vifaranga kutotoleshwa ndani ya siku moja wapewe glucose kwa muda wa masaa mawili. Glucose huchanganywa katika maji na kupewa vifaranga hawa na baada ya hapo vifaranga wapewe mchanganyiko wa vitamins mfano ni AMINOVIT na OTC plus


Pia hii huchanganywa na maji. Vifaranga wawekwe katika eneo lenye joto wastani na safi. Baada ya hapo siku ya pili na kuendelea vifaranga wapewe 



2.       SIKU YA 7. 
vifaranga wapatiwe chanjo ya NEWCASTLE (KIDERI). chanjo hii huchanganywa na maji safi katika eneo lenye kivuli kIsha kupewa vifaranga kwa muda wa masaa mawili kisha toa maji hayo na kuyamwaga mbali na eneo ambalo kuku wengine wanaweza kuyafikia,au kuyachimbia.baada ya hapo vifaranga wapewe maji yenye mchanganyiko wa vitamini 
3.     SIKU YA 14. 
Wapewe chanjo ya GUMBORO(IBD). Chanjo hii pia huchanganywa katika maji na kupewa vifaranga kwa muda wa masaa mawili tu, baada ya hapo vifaranga wepewe mchanganyiko wa vitamin. Kuku waliokufa kwa ugonjwa huu unaweza kuwatambua kwa kuchana vifua vyao na hapo utaona vidoti vyekundu kama hapo pichani
4.     Siku ya 21 (wiki ya tatu) 
Rudia chanjo ya Newcastle (Kideri) 
5.     SIKU 28 (Mwezi) 
Rudia chanjo ya GUMBORO IBD 
6.     SIKU 35 (Mwezi 1 na wiki 1) 
Kipindi hiki kuku wapewe mchanganyiko wa vitamin ya kutosha. 
7.     WIKI YA 6-8 
KUKU wapatiwe kinga ya Ndui (fowl pox).kinga hii sio rahisi kwa mfugaji asiye na utaalam kuwapa kuku, tafuta mtaalum wa mifugo kwa kazi hii au upate maeleze ya jinsi ya kuweka kinga hii.
8.    WIKI YA 8 

Kuku wapatiwe dawa ya minyoo kama Piperazzine na baada ya hapo unaweza kurudia chanjo ya Newcastle
Share:

DIAMOND KAYAZUNGUMZA HAYA KUHUSU MIMBA YA HAMISA


Mwimbaji wa Bongofleva kutoka WCB Diamond Platnumz amefunguka kuhusu story ambayo ilimake headline akidaiwa kuwa mapenzini na Hamisa Mobetto ambapo inadaiwa amempa ujauzito Mwanamitindo na kuonekana kuwa karibu na mama yake Diamond.
Diamond amesema hakuwai kuwa na uhusiano na Hamisa akisema hafahamu lolote kuhusu ujauzito bali ni story anazozisikia tu:>>>“Kuhusu mimba ya Hamisa mimi sijawahi kuwa na mahusiano naye. Hizi ni stori ambazo kila siku hata mimi nazisikia.
“Toka nimefanya na Hamisa Mobetto video ya Salome watu wameongea kweli lakini mimi sina mahusiano naye.” – Diamond Platnumz.
Share:

FAHAMU UFUGAJI BORA NA WAKIBISHARA WA KUKU WA ASILI



Ufugaji wa kuku wa asili ni nyenzo muhimu katika kupambana na wimbi la umasikini kwa kuongeza kipato cha kaya. Hata hivyo, pamoja na soko la uhakika, bado ufugaji kuku haujaweza kutumika ipasavyo kupambana na umaskini unaowakabili Watanzania wengi. Ni mazoea kwa jamii nyingi hapa Tanzania kufuga kuku wa asili kama sehemu ya mila na desturi zao. Kuku wa asili amekuwa akifugwa bila ya kupatiwa huduma muhimu kama makaazi bora, chakula cha ziada, tiba, kinga za magonjwa mbali mbali. Muhtasari huu unatoa muongozo wa ufugaji wa kuku wa asili ili uweze kuzalisha na hatimae kukuza kuku kwa wingi.
 http://ufugajimakini.blogspot.com/
Dondoo ya 1
Usafi wa vyombo na mazingira ya kuku
Uchafu ni mama wa magonjwa, hivyo zingatia haya;
1.  Vyombo vya chakula na maji visafishwe mara kwa mara kwa maji safi na sabuni.
2.  Pumba au chakula kilicholowana na kuchanganyika na kinyesi cha kuku kitolowe na kufukiwa.
3.  Choma moto au zika kwenye shimo refu kuku waliokufa kwa ugonjwa.
4.  Usifuge kuku na ndege wa jamii nyingine kwa mfano bata katika banda moja.
5.  Ondoa mbolea mara kwa mara kutoka katika banda la kuku.
6.  Tumia dawa za kuulia vimelea kusafishia banda na upake chokaa angalau mara moja kwa mwaka.
7.  Ziba matundu yote yanayoweza kuruhusu panya na wanyama wakali kama vicheche kuingia katika banda la kuku.
Dondoo ya 2
Magonjwa na kinga kwa kuku wote
Ndui ya kuku
Huathiri sana vifaranga wanaokua na ujitokeza kwa wingi wakati wa mvua za muda mrefu. Husababisha vivimbe katika uso/ kishungi na hata sehemu nyengine zisizo na manyoya.
Mdondo/kideri
Mdondo, au kwa majina mengine lufuo, au kideri ni ugonjwa hatari katika magonjwa ya kuku wa asili. Ni ugojwa wa virusi ambao huathiri kuku wa rika zote, huweza kuangamiza kuku wote kijijni.
Ukosefu wa vitamini A
Ugonjwa huu husababisha macho kuvimba na kutoa uchafu mziito kama sabuni iliyolowana. Kuku wenye dalili hizi hawaponi na hata kufa. Ugonjwa hujitokeza baada ya kipindi kirefu cha kiangazi kwa ajili ya ukosefu wa majani mabichi.
Kosidiosisi
Huathiri kuku wa umri wowote lakini huuwa zaidi vifaranga na kuku wanaokua. Kuku hudhoofika, manyoya huvurugika na kuku huwa kama wamevaa koti. Kuku huarisha damu au kinyesi cha kahawia na huzubaa na kuonekana kama wamevaa koti.
Viroboto, chawa na utitiri
Hawa ni wadudu wa nje wanaoshambulia ngozi. Huweza kusababisha ugonjwa kutokana na kunyonya damu. Viroboto hushambulia kichwa na kunata huku wakinyonya damu. Viroboto huuwa vifaranga. Chawa na utitiri hughasi kuku hadi wakashindwa kutaga na kuatamia.
Minyoo
Minyoo huweza kudhofisha kuku na kuwafanya waweze kuugua maradhi mengine kirahisi. Muone mtaalaam ukihisi kuku wako wana minyoo.
Dondoo ya 3
Chakula cha ziada
1.  Wapatie vifaranga nyongeza ya protini kwa kuwachanganyia vumbi la dagaa au vichwa vya dagaa vilivyotwangwa kwenye pumba za mahindi.
2.  Changanya kikombe kimoja cha vumbi la dagaa na vikombe vitano vya pumba za mahindi (tumia kikombe kidogo cha chai).
3.  Mchwa na wadudu wengine wanaweza kutumika kama nyongeza ya protini.
4.  Vuna mchwa kwenye vichuguu au tengeneza mchwa katika njia za mchwa.
5.  Kutengeneza mchwa: changanya kinyesi cha ng’ombe na majani makavu, mabua ya mahindi au maranda ya mbao katika chungu au ndoo ya zamani.
6.  Mwagia maji hadi kila kilichomo kilowane kisha weka katika chombo kama ndoo au chungu. Weka chombo chako katika njia ya mchwa ukikigeuza juu chini na subiri hadi kesho yake asubuhi, kisha beba vyote vilivyomo na uwamwagie kuku mahali walipo.
Dondoo ya 4
Utotoleshaji wa vifaranga
Chagua jogoo bora na tetea bora kuzalisha kuku.
Sifa za jogoo bora
1.  Awe na umbo kubwa, awe ukiko mzuri na usioangukia upande mmoja.
2.  Apende kuwa na himaya yake. Ukimpata jogoo mwenye sifa hizi mueke yeye na matetea kumi. Hivyo ukiwa na matetea ishirini jogoo wawili wanatosha.

Sifa za tetea bora
Tetea bora ni yule mwenye umbo kubwa, mwenye uwezo wa kutaga mayai ya kutosha, kuatamia na hatimaye kutotoa vifaranga.
Uhifadhi wa mayai
1.  Weka mayai mahali safi na penye hewa ya kutosha.
2.  Tumia kasha lililokatwa na kujaza mchanga mkavu na safi au kasha la kuhifadhia mayai.
3.  Weka sehemu butu ya yai iwe upande wa juu na ile iliyochongoka itizame chini.
4.  Andika namba au tarehe katika siku lilipotagwa.
5.  Mayai yakishatagwa yatolewe na kuhifadhiwa na moja liachwe kwenye kiota ili kumuita kuku kuja kutaga kesho yake.
Kuatamiza mayai
1.  Kuku awekewe mayai yatakayokuwa na uwezo wa kuyaatamia na kuyatotoa yote.
2.  Mayi 10 hadi 12 yanatosha kuatamia.
3.  Mayai ya kuatamiza yasizidi wilki 2 toka kutagwa.
4.  Yai la mwisho kutagwa liwe la kwanza kuchaguliwa hadi yapatikane mayai 10 mpaka 12, na apewe kuku wa kuyaatamia.
5.  Mayai ya kuatamiza yasafishwe kwa kitambaa kikavu na safi au kilichowekwa spiriti
Kutotolesha vifaranga wengi kwa wakati mmoja
1.  Kama unataka kuku zaidi ya mmoja watamie na kutotoa kwa mpigo fanya yafuatayo;
2.  Kuku wa kwanza akianza kuatamia muwekee mayai yasiyo na mbegu mfano mayai ya kuku wa kisasa au kuku asiye na jogoo.
3.  Rudia zoezi hilo hadi utakapofikisha kuku watano kisha wawekee kuku wote mayai yenye mbegu.
Dondoo ya 5
Matunzo ya vifaranga ili kuzuia vifo
Vifaranga wengi hufa kabla ya kufikisha miezi miwili kutokana na magonjwa, baridi na kuliwa na wanyama wengine. Ili kupunguza vifo vya vifaranga wa siku 1 hadi miezi miwili zingatia yafuatayo;

Ulinzi dhidi ya mwewe na wanyama wengine
1.  Weka vifarang kwenye tega na kuwafunika ili wasinde mbali wakati wa mchana. Wape maji na chakula. Hakikisha hawapigwi jua wala kunyeshewa mvua. Wakati wa usiku walale na mama yao.
Chanjo ya mdondo kideri/lufuo
Kama tetea alichanjwa kabla ya kuanza kutaga vifaranga wanaoanguliwa huwa na kinga ya mdondo ya kuwatosha kwa wiki 3 za kwanza za maisha yao. Wachanje vifaranga hao dhidi ya mdondo wafikishapo umri wa siku 18.
Vifaranga ambao historia ya chanjo ya mama haijulikani, wapewe chanjo ya mdondo siku tatu baada ya kuanguliwa, rudia hadi wakifikisha wiki tatu kisha uchanje kila baada ya miezi 3
Kinga dhidi ya kosidiosisi
Kinga ya kosidiosisi kwa vifaranga, itolewe hata kama ugonjwa haujajitokeza.
1.  Wape dawa ya amprolium kwa muda wa siku tatu mfululizo mara wafikishapo siku saba tokea waanguliwe kama kinga ya kosidiosisi.
2.  Dawa inaweza kutolewa hata kama wamevuka umri huo. Fuata maelekezo ya mtaalam juu ya kiasi cha dawa kinachopaswa kuchanganwa katika maji au pumba
3.  Kama vifaranga wadogo wataonesha dalili za kuzubaa kama kuvaa koti wapewe dawa ya amprolium kwenye maji kwa utaratibu ufuatao;
Dawa siku tatu mfululizo: usiwape kwa siku mbili; gawa tena kwa siku tatu

Hitimisho
1.  Hakikisha banda na vyombo vya chakula cha kuku ni visafi kuepusha magonjwa.
2.  Usichanganye kuku na bata katika banda moja
3.  Lisha chakula cha ziada hasa kwa vifaranga.
4.  Kideri, kosidiosisi, ndui na upungufu wa vitamini A ni vyanzo vikuu vya vifo vya kuku wako. Kumbuka kukinga kuku wako dhidi ya magojwa haya.
5.  Kumbuka kuchagua mayai ya kuatamiza kama ilivyoelekezwa ili kuepuka kupata mayai viza.
6.  Vifaranga wadogo hadi wiki nane huhitaji matunzo mazuri, fuata maelezo kuzuia vifo.
7.  Kumbuka ukiuza kuku wengi kwa mpigo utaongeza mapato yako, jitahidi kuzalisha vifaranga kwa wingi ili upate kuku wengi baadae.
8.  Muone mtaalam wa mifugo ulie karibu nae kwa ushauri zaidi.
9.  Soma maelezo haya mara kwa mara na ufanye yalioelekezwa.
10.              Washirikishe wengine katika kaya yako ili nao wajifunze na kufanya hivyo kukuza ufugaji na kipato cha familia.

Share:

DRONE CAMERA KWA BIE POWA

tomtop.com INT

PHONES

tomtop.com INT

.

https://ad.admitad.com/shuffle/45eb471090/

.

Total Pageviews

PATA SIMU NZURI KUTOKA NJE

Aliexpress INT

Labels